Mengi adai waziri ataka kumuhujumu..
Hivi karibuni waziri mmoja kijana anayeongoza wizara nyeti alipendekeza nibambikiziwe kodi bandia ya kiasi kikubwa nitakachoshindwa kulipa na hatimaye nifilisiwe kama njia pekee ya kuninyamazisha kabisa eti kama alivyofilisiwa tajiri mmoja mkubwa huko Urusi.
Alidai kwamba vyombo vyangu vya habari vimekuwa mno mstari wa mbele kupiga vita ufisadi, jambo ambalo kwa maoni yake siyo zuri kwa sababu linawanyanyasa baadhi ya watu.
Nilitegemea waziri huyo msomi sana angefahamu jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi. Angalao angefahamu kwamba anayeamua nini kiandikwe na nini kisiandikwe ni mhariri wa gazeti ambaye taaluma yake ni uandishi wa habari na siyo mmiliki wa vyombo vya habari.Kama mkiristo na kama alivyoagiza Bwana Yesu namsamehe kwa vile hajui atendalo.
Baada ya kumsamehe ningetaka ajue yafuatayo.Asiyekemea maovu katika jamii, yeye ni sehemu ya maovu hayo. Waziri huyu na wale wote ambao wamekwishanitumia vitisho wakumbuke kwamba hata kama watafanikiwa kuvinyamazisha kwa hujuma zozote zile, vyombo vyangu vya habari, na hata kama mimi sitakuwepo tena, moto wa kupiga vita ufisadi uliokwishawashwa katika akili za wanajamii hauwezi kuzimika kamwe.
Ieleweke pia kwamba sauti za maskini na wanyonge katika jamii hazisikiki kwa urahisi. Vyombo vya habari husaidia kupaaza sauti na vilio vyao katika vita dhidi ya maovu. Ni wajibu wa kila mtu aliye na uwezo kusema kwa sauti kubwa kwa niaba ya wanyonge na maskini ili kutokomeza ufisadi.
Nachukua fursa hii kumpongeza sana Rais wetu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuguswa na sauti na vilio vya wanyonge na maskini wa Tanzania kuhusu ufisadi na hatua za kijasiri zinazochukuliwa na Serikali yake dhidi ya ufisadi.
Sisi sote ni lazima tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azidi kumpa ujasiri, nguvu na hekima nyingi wakati huu wa majaribio makubwa.