Friday, November 28, 2008

Baada ya Obama Afrika kupata rais mweupe?



NELSON Mandela alikuwa Rais mweusi wa kwanza Afrika ya Kusini, na watu wote wapenda amani walifurahi na kuamini kuwa sasa ubaguzi wa rangi umekwisha na watu weusi ambao ni wengi watafaidi matunda ya harakati zao.

Walitarajia maisha bora kwa wote na uchumi wa nchi kuwanufaisha wote. Sisi pia tuliposaini mikataba ya ushirikiano wa kibiashara tulidhani tutaona weusi wengi wenye uwezo wa kifedha, elimu na viwanda watatusaidia sisi tuliojitoa mhanga kwa ajili yao.

Hatukujaliwa kukumbuka kuwa mfumo wa ukoloni mkongwe, ubepari na ubaguzi uliotawala nchi hiyo kwa miongo mingi haukuwa umemtayarisha mtu mweusi kushika hatamu za uchumi kwa hiyo siasa na jamii. Matokeo yake wengi wana uchungu wa kuona “kaburu” kahamia Tanzania na ana kula kuku kwa mrija kwa jina la ushirikiano wa kibiashara.

Leo hii watu weusi wa Afrika ya Kusini hawana tafauti na wenzao Kaskazini ya mto Limpopo ambao tulipata uhuru wa bendera tu.

Sasa tumepata Rais mweusi mwingine wa kwanza katika Marekani! Kwa vile fungate la ushindi huo limekwisha, inabidi tuanze kujiuliza maswali magumu: Je hii ina maana gani kwetu? Waamerika wenyewe wanajigamba kuwa uchaguzi huo ni mfano wa kiwango cha juu cha demokrasia popote.

Ni kweli, kama ambavyo Rais Bush ni Rais wa Marekani, na si Rais wa Marekani mwenye asili ya Ulaya, Obama naye anaitwa Rais mteule wa Marekani, na si Rais Mteule wa Marekani mwenye asili ya Afrika.

Kwa hiyo, kisaikolojia mtu mweusi kapanda hadhi kidogo kwa kutambuliwa kuwa ni raia kamili wa Marekani.

Ila kwa nini iwe hivyo sasa? Ni kweli kwamba demokrasia ya Marekani imekomaa hasa wakati huu inapojenga himaya yake duniani kote au kuna jingine? Nini athari ya demokrasia ya Marekani kwa Afrika?

Kwa tathmini yangu, hasa nikiangalia miaka kadhaa ijayo naona kuna ajenda. Kwanza ni ile dhana ya utandawizi kwamba dunia sasa ni kijiji kimoja na ye yote mwenye nia, ari, uwezo anaweza akawekeza popote na hata kutawala katika nchi kama Marekani!


Obama
Obama

Obama, ambaye babake ni Mkenya lakini yeye ni Mmarekani, ameweza kufanikiwa kupata cheo kikubwa duniani, tena akiwa na umri mdogo kabisa. Kwa maana hiyo, wapo weupe wengi waliozaliwa na kukulia Afrika; yaani Wazungu, Waarabu, Wahindi, Wachina na wengine. Kwa sasa tunao marais weupe Afrika, lakini wanaishia katika nchi za Afrika ya Kaskazini.

Tukifuata demokrasia ya Marekani ni kwamba kuna siku bara la Afrika litapata marais wengi weupe. Na hawa wataiunganisha Afrika ili ipate Rais mmoja.

Naweza nikaonekana naota ndoto ya alinacha; lakini kwa jinsi dunia inavyokwenda, suala hili si ndoto.

Kwa mfano tukishindwa kulipa madeni na kutangazwa mufilisi, mweupe mmoja kama Bill Gates au Mfalme wa nchi za Kiarabu anaweza akatununua kwenye mnada tu! Wakubwa wanajua Waafirka hatujawahi kuwatawala na kuwanyanyasa mataifa mengine katika nchi zao, kwa hiyo ni rahisi kwa mtwana kuwa “bwana”. Lakini wao kuja kututawala sisi huo utakuwa ni ukoloni au utumwa kujirudia!

Kuna wanao dai kwamba Obama ni kizazi kipya cha Waafrika, kwa vile baba yake hakutokana na kizazi kilichochukuliwa utumwa. Ukweli unabaki palepale: hizo ni propaganda za kutugawa ili wengine wajione bora kuliko wengine. Mtu mweusi popote duniani ni taifa lililonyanyaswa kuliko yote katika historia, na wote ni waathirika na waadhirika wa biashara dhalimu ya utumwa hadi leo!

Hebu fikiria Afrika ya Kusini au Kenya ipate Rais mweupe leo, itawezekana? Ilichukua karne nyingi kwa ngozi nyeusi kukubalika huko Marekani, lakini kwa ajili ya tabia yetu ya kusahau haraka itachukua muda mfupi kujiona sie tunakubalika sasa.

Na kwa vile hilo linajulikana na wakubwa, ndio maana zinatafutwa njia za mkato kama Obama, au pengine baadae Serikali ya Obama inaweza kuweka mkwara kutubana; tuwe na kipengele katika sheria za uchaguzi kisichobagua mtu kwa rangi yake kugombea nafasi kubwa kama urais kama tuna taka msaada.

Naamini kwa dhati raia wa Marekani waliopiga kura katika Uchaguzi wao mkuu uliopita walipigia kura mabadiliko. Waliamini serikali itakayoongozwa na chama cha Democrats, chini ya uongozi wa Rais mteule Obama, iko katika nafasi nzuri ya kuleta mabadiliko yanayotakiwa na wengi.

Swali kubwa ninalojiuliza: Obama ameweka wazi kwamba yeye ni Mmarekani na maslahi ya nchi yake yanakuja kwanza; je kuna tafauti gani kati ya Democrats na Republicans?

Kimsingi vyama hivi vikubwa Marekani vyote vinaweka maslahi ya Marekani kwanza, tafauti yao ni katika mbinu za utekelezaji. Naweza kufananisha Republicans na simba anaenguruma na kuonekana kwa urahisi na kutisha. Democrats ni nyoka ambaye huwezi kujua kwa urahisi kama yupo mpaka akung’ate.

Mbinu za Republicans ni za kibabe kama zile za polisi anayekupa mikong’oto ili umpe taarifa anayoitaka, ukiwa karibu kufa anakuja polisi mwema ambaye ni Democrat na kukwambia bora uongee na yeye!

Huyu (Democrat) anakuja kwa upole na kirafiki na maji atakupa na kusema yule jamaa hana msalie Mtume, bora umweleze yeye kila kitu; kisha yeye atajua namna ya kukusaidia. Kwa hiyo wakati Republicans wanatumia nguvu na ubabe, Democrats wanatumia diplomasia, lakini lengo linabaki palepale - maslahi ya kwanza ni kwa Marekani .

Je ni nani wanaamua na kudhibiti maslahi ya nchi? Katika kitabu chake “The secret history of the American Empire”, toleo la 2007, mwandishi John Perkins anasema: “Hawa wanaume na wanawake (waumini wa utawala unaoongozwa na wafanyi biashara wakubwa anao waita corporatocracy) ndio wanaoongoza nchi, hawajali ni chama gani kiko Ikulu au kina wabunge wengi bungeni.

Hawaguswi na matakwa ya umma, na hakuna sheria inayowapa kikomo cha kuongoza.” Na ndio wanaojenga Himaya ya Marekani, The Empire, yaani taifa kubwa kiuchumi, kijeshi na kisiasa.

Kwa nini walimwengu wanaifananisha Marekani na himaya kama zile za Warumi, Waingereza na wengine?

John Perkins ni Mmarekani ambaye alitumikia shirika la kimataifa lililotoa ushauri wa kupotosha uchumi wa nchi “masikini” za Asia, Marekani ya Kusini na Afrika kwa niaba ya himaya ya Marekani. Yeye na kundi la wataalamu wenzake walizishawishi nchi mbalimbali kukubali mikopo mikubwa kwa ajili ya maendeleo kama vile miradi mikubwa ya umeme, barabara, viwanja vya ndege, bandari na miji ya kisasa inayofanana na Marekani!

Kazi yao nyingine ilikuwa kuhakikisha kwamba mikataba ya miradi hiyo inaenda kwa kampuni za Kimarekani. Nchi hizi zikishaelemewa na madeni ndipo Serikali ya Marekani inakuja na mikakati ya kudai madeni kwa kutaka rasimali zenu au ushirikiano katika masuala ya kijeshi na siasa.

Matokeo yake ni nchi hizi kuendelea kufukarika na hivyo serikali kushindwa kutoa huduma muhimu kwa raia wake kwa vile inalipa madeni ambayo hayaishi; kwani yalikuwa ni mtego wa kifo.

Perkins anasema kwamba kama wao wakishindwa kuishawishi nchi ikubali kwa hiyari ya lazima, basi nchi hizi, ama huvamiwa kijeshi, au huyo kiongozi hupinduliwa na kibaraka kuingizwa madarakani.

Kwa sifa zake hizo na nyingine, Marekani inaitwa “Himaya” kwa vile ina vigezo vyote vya “Himaya”. Kwa mfano, kiu isiyoisha ya kutaka kutawala wengine na kunyonya rasilimali zao. Aidha ina ulafi wa rasilimali nyingi zaidi ukilinganisha na nchi zingine, na inakuwa na jeshi kubwa sana kuimarisha sera zake.

Hulka ya himaya yoyote kama Marekani ni kueneza lugha yake, fasihi, sanaa na utamaduni wake; hasa ule wa hovyo kwa makoloni yake. Huwatoza kodi hata watu ambao si raia wake katika nchi zingine. Hulazimisha kutumika sarafu na baadhi ya sheria zake kwa nchi zingine.

Perkins anasema kwamba Marekani ina sifa hizo zote. Kwa mfano, idadi ya watu wa Marekani ni asilimia tano (5%) ya watu wa dunia nzima, lakini inatumia zaidi ya asili mia ishirini na tano (25%) ya rasilimali za dunia nzima! Imefanikiwa katika hilo kwa kuzinyonya nchi zingine zenye uchumi unaokua.

Pamoja na kwamba himaya hii imejekengeka kwa njia za kiuchumi, lakini viongozi wote duniani wanajua njia zote zikishindikana jeshi lake kubwa na la kisasa litatumika. Kwenye himaya za zamani kulikuwa na watawala maalumu wakiitwa “Emperor” au Mfalme ambao hawakuchaguliwa kwa kura za watu wala hawakuwa na ukomo wa kutawala. Hawa walidhibiti serikali, jeshi na vyombo vya habari.

Marekani ina kundi la watu ambao wanatawala kwa pamoja mithili ya mfalme. Watu hao wanaendesha makampuni makubwa na kupitia hayo makampuni wanaendesha serikali, anasema John Perkins.

Na kwa vile wanafadhili kampeni za kisiasa na vyombo vya habari, wana uwezo mkubwa wa kuwadhibiti viongozi waliochaguliwa ikiwa ni pamoja na kuamua ni taarifa gani raia wazipate katika vyombo vya habari.

Ndio maana si ajabu Wamarekani wengi hawajui ukweli kuhusu nchi yao nje ya mipaka yao, na sisi hatujui mengi kuhusu Marekani; hata kama tunaangalia CNN saa zote!

Kwa kiasi kikubwa yaliyomo kwenye katiba ya Marekani - haki za watu na maneno mengi kuhusu demokrasia hayaendani na vitendo vyao wanapoangalia maslahi ya nchi yao.

Sasa hiyo ndio nchi ambayo Obama anatarajia kuiongoza baada ya kuapishwa rasmi! Sifa na heshima ya himaya hii iko chini na watu wengi duniani sasa wamechoshwa nayo; japo hawajui la kufanya.

Je Rais Mteule Obama ataweza kuleta mabadiliko ya sera za nje bila kuhatarisha maslahi ya himaya ya Marekani? Je huko ambako imeleta uharibifu, madhara na madhila, na watu wanajua ni kwa sababu ya sera za Marekani, atafanya nini?

Huku kwetu (Afrika) kwenye maliasili nyingi kama mafuta na madini na ukanda mkubwa wa bahari, kuna tishio la Marekani kuweka vituo vya kijeshi vya Africom. Je Obama ataendeleza mpango huo? Je Marekani, ambayo inatumia mabilioni ya mapesa, rasilimali watu na muda kutengeneza silaha za mauaji ya halaiki, itaweza kufunga na kuviteketeza viwanda vyake haramu na kutafuta njia mbadala ya kupata pesa? Rais Mteule Obama ataweza kupambana na watemi wa vita?

Rais Mteule atachwa atawale na kuongoza na kuleta mabadiliko au atatumiwa kama Afisa Uhusiano wakubadilisha taswira ya Marekani kwa walimwengu ?

Haya ni baadhi ya maswali tunayopaswa kujiuliza katika kipindi hiki ambacho Rais Mteule Obama anasubiri kuingia rasmi Ikulu ya Marekani kuanza kazi.

Article source;www.raiamwema.com

WEEKEND NJEMA

Mwaka 2008 upo mbioni kuelekea ukingoni mwake.Zimebaki wiki kadhaa tu kabla hatujaona zile fataki hewani na kusikia ving’ora vikitusindikiza kuumalizia mwaka.Kwa vyovyote vile mwaka 2008 utaenda na historia kadhaa zenyewe kuvutia kwa wengine na kutia simanzi kwa wengine.Ndio maisha.Ni mwaka ambao hakuna atakayeweza kamwe kusahau kwamba mtu mweusi wa kwanza amechaguliwa kuliongoza taifa kubwa la Marekani.

Lakini nchini kwetu pia ni mwaka ambao tunaweza kusema tumeshuhudia mengi ambayo siku za nyuma yalionekana kuwa hayawezekani.Tumeona viongozi kadhaa wakijiuzulu nyadhifa zao.Tumeshuhudia wengine wakipandishwa kwenye karandiga.Tumeona wazee wengine wakipandwa na pressure kwa sababu wanajua walishaharibu na hawana uhakika na kesho.Nadhani tunakubaliana kabisa kwamba miaka kadhaa ya nyuma,ilikuwa ni kama ndoto kusikia kiongozi akitangaza kujiuzulu.Mifano ya waliowahi kujiuzulu ilikuwa ni michache sana.

Inawezekana ni “changa la macho” na kwamba kinachofanyika ni mchezo wa aina yake wenye wingu zito la kisiasa.Inawezekana kabisa(hakuna lisilowezekana katika dunia hii).Lakini pamoja na yote hayo,tofauti na siku za nyuma,hata kile kitendo tu cha kuwaona waheshimiwa wakitokwa na jasho kwa sababu hawamo ndani ya yale “mashangingi” yao na badala yake wamekalia yale yale mabenchi ambayo hawakuwahi kuona umuhimu wa kuyakarabati kwa sababu “hayakuwahusu” na huku wakiwa wameegemea zile kuta ambazo hela yake ya rangi waliipeleka kusipotakiwa,ni vitu ambavyo vinaufanya mwaka 2008 uwe na lake katika historia.Bado tunasubiri kuona jinsi “changa la macho” litakavyopelekwa.Tupo na tunatizama kwa makini.Anayedhani tumelala anajidanganya.

Weekend njema!!

source-www.bongocelebity.com