Tuesday, December 23, 2008

MAHARAGE: Chakula bora kwa wenye presha, kisukari
BAADHI ya watu hawapendi kutumia maharage kama mboga kutokana na kuonekana kama ni mboga ya kimasikini, lakini kiafya maharage ni miongoni mwa mboga zenye faida kubwa mwilini na hutoa ahueni kubwa kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kama tutakavyoona leo katika makala haya;
Kwa mujibu wa utafiti mbalimbali, maharage, hasa yale meusi, ni chanzo kizuri cha kirutubisho aina ya ‘faiba’ kinachoshusha kiwango cha kolestro mwilini. Vile vile kiwango cha ‘faiba’ kilichomo kwenye maharage meusi, huweza kudhibiti kiwango cha sukari kisipande haraka baada ya chakula, hivyo kufanya maharage kuwa lishe nzuri kwa wagonjwa wa kisukari na shinikizo la juu la damu.
Iwapo utapata mchanganyiko wa maharage meusi na ule mchele ‘mweusi’ ambao haujakobolewa na kuondolewa virutubisho vyake muhimu (brown rice), basi utaweza kupata kiasi kikubwa cha protini na faiba ambacho huwezi kupata kutoka katika chakula kingine.
Aidha, utafiti wa muda mrefu uliofanywa na jarida moja lijulikanalo kama ‘Journal of Agriculture and Food Chemistry’, unaonesha kuwa mbali ya maharage kuwa na kiwango kikubwa cha ‘faiba’, pia maharage yana virubisho vingine vinavyojulikana kama ‘anthocyanins’ ambavyo hutoa kinga mwilini (antioxidant). Kiwango cha virutubisho hivyo kilichomo kwemye maharage, kinaelezwa kuwa ni kikubwa kuliko hata kinachopatikana kwenye matunda kama zabibu ambayo inaaminika kuwa na kiwango kikubwa zaidi.
Inaelezwa pia kuwa, watafiti walipofanya tathmini ya ziada kwenye maharage, waliweza kubaini kuwa maharage yanapokuwa meusi zaidi, ndivyo ambavyo kiwango kikubwa cha kinga kinavyoweza kupatikana, yakifuatiwa na maharage ya rangi nyekundu, kahawia, njano na mwisho meupe. Hii ina maana kwamba maharage meusi ndiyo yana virutubisho vingi zaidi kuliko maharage meupe na rangi nyingine.
Kwa ujumla, kiwango cha kinga (antioxidant) kilichomo kwenye maharage meusi ni mara kumi ya kile kinachopatikana kwenye matunda kama machungwa, zabibu na mengine. Hivyo unapokula maharage, siyo tu unapata ‘faiba’ ya kutosha bali pia unapata virutubisho muhimu mwilini kwa ajili ya kutengeneza kinga ya mwili dhidi ya vinyelezi vya maradhi.
Yafuatayo ni baadhi ya matatizo ya kiafya yanayoweza kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa na ulaji wa maharage meusi kama ilivyothibitika katika tafiti mbalimbali za kisayansi;
MAHARAGE YANA KINGA DHIDI YA SARATANI Utafiti umefanyika na kuthibitisha kuwa maharage meusi yana uwezo wa kutoa kinga mwilini dhidi ya saratani za aina mbalimbali.
MAHARAGE KINGA DHIDI YA UGONJWA WA MOYO Utafiti ulionesha pia watu wanaokula chakula chenye kiwango kingi cha ‘faiba’ kama vile maharage, hawako hatarini kupatwa na magonjwa ya moyo, ikiwemo kiharusi.
MAHARAGE HUONGEZA NGUVU MWILINI Ulaji wa maharage meusi husaidia kurejesha madini chuma mwilini na hivyo kuupatia mwili wako nguvu.
MAHARAGE YANA PROTINI NYINGI Maharage yana kiwango cha juu cha protini bora mwilini, hivyo badala ya nyama nyekundu, ambayo ikizidi ina madhara mwilini, kula maharage meusi.
Hizo ndiyo faida za maharage mwilini ambazo kila mtu anapaswa kuzijua kwa faida ya afya yake ya sasa na ya baadae.

No comments: